MTANGAZAJI

MEDIA INAPODHIHAKI SHIDA ZA WATU KWENYE SIKU YA WAJINGA


LEO NI SIKU YA WAJINGA, hata hivyo, ninachoandika hapa si utani wa Siku ya Wajinga. Ni jambo linalonikera, naamini, tuko wengi tunaokerwa juu ya namna media ya Tanzania inavyoitumia Aprili Mosi kuwasumbua wananchi wengi kwa utani unaowapelekea wananchi hao , wengi wao wakiwa na unyonge wa kiuchumi, kutaabika zaidi. Hii ni cynicism kutoka upande wa media.


Nitoe mifano michache; asubuhi hii Redio Country FM hapa Iringa imekuja na taarifa yenye kuwataka wananchi kuitikia ‘ofa’ iliyotolewa na Redio hiyo kwa watu kusafirishwa kwenda Loliondo kwa Babu juma lijalo. Kwamba watu hao waripoti kwenye ofisi za redio hiyo ifikapo saa nne asubuhi. Masikini, kuna wataohangaika kuiwahi ‘ ofa’ hiyo.Cynicism.


Televisheni ya Channel Ten wao wamewataka vijana wafike kwenye ofisi zao ifikapo saa nne ili wafanyiwe usahili kwa kazi ya utangazaji. Masikini, katika kipindi hiki cha mahangaiko ya vijana kutafuta ajira, kuna walio kwenye Daladala asubuhi hii kuwahi zilipo ofisi za Channel Ten. Cynicism.


Na magazeti nayo hakubaki nyuma. Kuna yaliyoripoti kuwa Babu wa Loliondo katua Dar. Lingine likachagiza kuwa Babu ameamua kutoa kikombe leo kwenye viwanja vya Jangwani. Kuna wagonjwa na wenye kuuguza wagonjwa watakaotaabika na taarifa hii. Cynicism.


Bila shaka kuna mifano mingine ya namna media inavyoitumia siku hii kudhihaki shida halisi za watu wetu walio wengi. Tabia hii ikemewe vikali. Si maadili mema.


Haya mambo ya kuiga kama Siku ya Wajinga yana wenyewe. Na wanapoyafanya wanatanguliza utu pia. Hata habari kuwa “ Kikombe Cha Babu” kinatibu UKIMWI na Saratani kwa wenzetu wangeisoma leo magazetini wangesema ni utani wa ‘ Siku ya Wajinga Uliokosa Ladha!|” Cynicism.



Media yetu inapaswa kuwa makini. Hili la kudhihaki na matatizo ya watu ikiwamo masuala ya afya linaweza kuwa na athari mbaya kwa media yenyewe. Watu wakakosa imani na media. Inatosha kwetu kusoma na kusikia mara kwa mara habari zinazofanana na za ‘ Siku ya Wajinga’.


Watu wakichanganywa zaidi na habari zisizo za kiweledi na utu katika siku kama ya leo, basi, watashindwa kutofautisha ipi ni habari ya kweli na ipi ya uongo hata katika siku za kawaida. Na huu ni ukweli wangu niliotaka kuusema. Ni mtazamo wangu .



Maggid

Iringa,
Aprili Mosi, 2011
http://mjengwa.blogspot.com

1 comment

Filipo Lubua said...

Bwana Maduhu,

Mimi niko pamoja nawe kupinga upotoshaji huu ambao unawaasiri watu wenye matatizo.

Sikatai wasiandike habari za kuwadanganya watu siku ya wajinga kama wanavyoiita. Hofu yangu zaidi ni pale wanapoleta 'ujinga wao' katika mambo yasiyo ya kijinga.

Unapomwambia mtu ambaye ni mgonjwa sana kuwa Babu wa Loliondo amefika Jangwani, na watu wakawatoa wagonjwa wao hospitalini kama walivyofanya huko nyuma, na wale wagonjwa wakaenda kufia hapo Jangwani, hili swala litakuwa la utani tena?

Hapa naona mjinga si yule aliyedanganywa bali ni yule aliyedanganya.

Kwa kweli vyombo vya habari vyatakiwa vijirekebishe sana, hasa katika maswala nyeti yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu

Mtazamo News . Powered by Blogger.